Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba amesema kuwa Serikali imelenga kupanda miti zaidi ya milioni 280 kila mwaka katika maeneo yaliyo katika hatari za kukabiliwa na hali ya jangwa na ukame.

Makamba amesema hayo leo wakati akiongea na Waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya kupambana  na kuenea kwa hali ya jangwa na Ukame Duniani inayofanyika tar 17 Juni kila mwaka.

“Ukataji wa miti kiholela na uharibifu wa misitu unaosababishwa na utegemezi  mkubwa wa binadamu wa kupata mahitaji kutokana  na mazao ya misitu pamoja na huduma zingine muhimu,kunazidisha ukubwa wa tatizo hili”, amesema Makamba.

Amesema Serikali imeandaa mkakati wa Taifa wa kupanda na kutunza miti wa mwaka 2016-2021 ambao unalenga kupunguza kasi ya uharibifu wa ardhi kwa njia ya kupanda na kutunza miti na kuhakikisha kwamba kila mwananchi  anahusika katika utaratibu huu.

Makamba amewataka wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kutekeleza kauli mbiu  ya mwaka huu isemayo ‘Ardhi ni Makazi yetu Tuitunze kwa manufaa ya baadaye

“Wananchi wote washiriki kikamilifu katika kuitekeleza ili kuhakikisha ardhi yetu inatunzwa kwa ajili ya kizazi kijacho”, amesema Makamba

Neno Kutoka Kwa Rais Wa TFF Kuelekea Uchaguzi Mkuu
Madega amvalia njumu Malinzi, atinga TFF