Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuenzi misingi ya utawala bora haitamvumilia kiongozi yeyote wa umma atakayekiuka misingi hiyo na kutanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma katika utendaji wake.

Amesema kuwa mgongano wa maslahi umechangia rasilimali za nchi kunufaisha watu wachache huku wananchi wengi kuendelea kuwa fukara, wakati wachache wakijitajirisha isivyo halali, hivyo Serikali itaendelea kuziba mianya.

Ameyasema hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika Kitaifa jijini Dodoma.

Aidha, amesema kuwa mgongano wa maslahi ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kuisababishia hasara Serikali kwa muda mrefu, tatizo ambalo lazima lidhibitiwe kwani mara kadhaa baadhi ya viongozi au watumishi wa umma wamekuwa wakifanya maamuzi kwa mambo wanayojua wazi kuwa wana maslahi binafsi nayo.

”Mathalani katika Halmashauri zetu wapo madiwani au watumishi wanaoshiriki kutoa maamuzi yanayo hitimishwa kwa kumpatia kazi mkandarasi au mzabuni wakati kampuni husika inamilikiwa na mwenza, rafiki, ndugu wa karibu au mtoa rushwa.”amesema Majaliwa

Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli itaendelea kuunga mkono na kutekeleza Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa ipasavyo. Mikataba hiyo ni pamoja na mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Makubaliano yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu.

 

Wabunge wawasilisha hoja kumng’oa Rais
EU yamuongezea vikwazo mshirika wa Kabila

Comments

comments