Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga amesema wataendelea na msako wa watu wanaowatumia walemavu katika vitendo vya kuwadhalilisha mpaka watakapohakikisha wahusika wanaofanya vitendo hivyo wanaacha kabisa.

Ummy amesema hayo wakati wa ziara yake ya kuwarejesha baadhi ya watu wenye ulemavu karibu 38 mkoani Shinyanga kutoka Jijini Dar es Salaam, kutokana na kundi hilo kutumiwa na watu wenye maslahi binafsi kuwazungusha watu wenye ulemavu kuomba fedha barabarani.

“Leo hii tumewarejesha watu wenye ulemavu zaidi ya 38 kutoka jijini Dar es Salaam kuja hapa mkoani Shinyanga mahali ambapo wamekuwa wakiishi hapo awali, hivyo kama rejista hiyo ingekuwepo basi zoezi la utambuzi wa baadhi yao ingekuwa rahisi kuwatambua, tutaendelea na msako hadi pale tutakapoona wahusika wa mtandao huu wanaacha kabisa vitendo hivyo vya udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu,” amesema Ummy.

Aidha, Ummy ameeleza kuwa serikali ipo katika mkakati wa kuandaa rejista ya watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, Halmashauri na Mkoa ili kuwa na takwimu sahihi zitakazoonesha idadi ya wenye ulemavu, kujua mahali walipo, wanajishughulisha na nini katika jamii waliyopo.

“Uwepo wa rejista hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa serikali kutambua idadi ya watu wenye ulemavu waliopo kwenye maeneo mbalimbali na hivyo kurahisisha ufikikaji wa huduma kwa kundi hilo kwa urahisi,” amesisitiza Ummy.

RC Shigela, ‘Natoa miezi miwili’
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Januari 11, 2021