Serikali imehaidi kufanya Maboresho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwemo kununua jenereta mbili kubwa ambazo zitatumika wakati umeme utakapokatika.

Kauli hiyo, imetolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dk. Pindi Chana katika mkutano wa majadiliano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma, uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Waziri huyo amesema moja ya marekebisho wanayotarajia kuyafanya ni kununua majenereta hayo ambayo yatasaidia kipindi umeme ukikatika na kuendelea kwa shughuli za michezo.

“Moja ya tukio ambalo tulipata matatizo makubwa ya kukatika kwa umeme ni mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, hivyo tutahakikisha tunaboresha lisijirudie tena,” amesema.

Pia, Waziri huyo amesema wizara hiyo ina mkakati wa kuendelea kuibua vipaji vya michezo shuleni na namna sekta hiyo itakavyopiga hatua.

“Michezo ni ajira na inakuza uchumi duniani, hivyo tunahitaji kuendeleza vipaji kuanzia ngazi ya chini,” amesema.

Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Said Yakubu amesema zaidi ya sh. bilioni 35 zimekusanywa kupitia sekta ya michezo kutokana mafanikio yaliyo patikana katika michuano mbalimbali.

Yakubu amesema sekta hiyo, imeanza kupiga hatua katika michezo kufuatia kuwepo baadhi ya wadhamini ambao wanadhamini michezo mbalimbali.

“Tuna mpango wa kuboresha mikopo kwa wasanii kwa kushirikiana na benki ili wadau hao wachukue fedha kupitia kwa benki ambazo tutakubalina nao,” amesema

TASAC yaelimisha Jamii utekelezaji wa majukumu kisheria
Viwango malipo ya Nyumba vyawaliza wakazi Magomeni kota