Serikali imesema kuwa iko katika hatua nzuri ya kukamilisha hatua za ujenzi wa bandari ya uvuvi na kununua meli kwa ajili ya kuvua samaki kwenye eneo la bahari kuu pamoja na kuziwezesha meli nyingine kutia nanga katika bandari hiyo ikiwa ni lengo la Tanzania kwenda sambamba na nchi nyingine duniani kukuza uchumi kupitia sekta ya uvuvi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega mara baada ya kuwasili nchini akitokea jijini Nairobi nchini Kenya, ambapo hivi karibuni alihudhuria mkutano uliowajumuisha wajumbe zaidi ya elfu nne, kutoka mataifa mbalimbali, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli aliwakilishwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.

Amesema kuwa mchango wa sekta ya uvuvi hapa nchini bado ni mdogo hivyo mkutano huo umeongeza hamasa kwa Tanzania kutafuta namna bora ya ukuaji uchumi kupitia sekta ya uvuvi.

“Sisi tuko katika hatua nzuri ya kuweza kukamilisha ujenzi wa bandari ya uvuvi, tukishafanikiwa kujenga bandari ya uvuvi, maana yake ni kwamba meli zitatia nanga hapa kwetu, tutapata ajira, tutatengeneza pia vile vile  maeneo ya kuhifadhia samaki kwa wingi, tutachakata, tutakuwa na uwezo wa kuuza katika soko la ndani na soko la nje.”amesema Ulega

Hata hivyo, Ulega ameongeza kuwa serikali imeshaanza hatua ya ununuzi wa meli zake zenyewe, hatua iliyoilazimu kulifufua Shirika la Uvuvi (TAFICO) ambalo tayari limeshaanza kufanya kazi.

 

Kilo moja ya Korosho yasababisha mwanafunzi kubakwa
Ligi ya mabingwa Ulaya: FC Barcelona yatinga 16 bora