Serikali imesema kuwa itatekeleza ahadi zote ilizowaahidi wananchi katika maeneo mbalimbali nchini hivyo imewataka kuendelea kutoa ushirikiano na kuiamini kwani imedhamiria kuwaletea maendeleo.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Songwe kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mkoani Songwe akiwa katika ziara ya kikazi.

Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya Tano ipo makini na imejipanga vizuri katika kutekeleza ahadi mbalimbali zilizotolewa na Rais Dkt. Magufuli kama Ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 inavyoelekeza.

“Ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. Magufuli tutazitekeleza, ikiwemo na hii aliyoikumbusha Mheshimiwa Mulugo ya ujenzi wa kilomita nne za barabara ya lami. Tunawaomba wananchi muendelee kuwa na imani na Serikali yenu.”amesema Majaliwa.

Aidha, Majaliwa amepiga marufuku wananchi kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji na kuwataka washirikiane katika utunzaji wa mazingira ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.

Vile vile amesema kuwa ni vema wananchi wakazingatia Sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu zikiwemo za kilimo kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa Kampeni ya Rais Dkt. Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, ambapo itahakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma ya maji katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Gallawa akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa huo amesema kuwa watu wanaopata huduma za maji safi na salama katika maeneo ya mijini ni asilimia 42 na vijijini ni asilimia 41.6.

 

LIVE: Rais Magufuli akizindua ujenzi wa barabara Kasulu, Kigoma
Jeshi la Polisi: Kibiti mambo shwari anayetaka kwenda kuishi ruksa