Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa Kanuni za taarifa za Usafirishaji na uingizaji wa fedha taslimu kutoka na kwenda nje ya nchi (Crossborder Declaration of Currency and Bearer Negotiable Instruments Regulations) ambapo wasafirishaji wa fedha taslimu na wasafiri wote wanaotoka au kuingia nchini, watatakiwa kutoa taarifa za fedha taslimu wanazosafirisha ikiwa fedha hizo zinalingana au zinazidi kiasi cha dola za kimarekani elfu kumi (USD 10,000).

Hayo yamesemwa na Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu, Onesmo Makombe wakati wa ufunguzi wa warsha ya utekelezaji wa Kanuni hizo, ambapo amesema utekelezaji wa kanuni hizo, pamoja na mambo mengine utaiwezesha nchi kuwa na takwimu za usafirishaji fedha taslimu.

“Takwimu hizo zitakazosaidia pamoja na mambo mengine kubaini vitendo vya kihalifu, kupunguza utoroshaji wa mitaji na kuhakikisha kuwa tunapunguza kama siyo kumaliza kabisa usafirishaji wa fedha zitokanazo na uhalifu au/na fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi” alisema Bw. Makombe

Amesema kuwa kanuni hizo zimeweka adhabu zitakazochukuliwa dhidi ya wale watakabainika kutaka kupita na fedha zinazolingana au zinazozidi kiwango kilichowekwa bila kutoa  taarifa au watakaotoa taarifa za uongo.

Hata hivyo, Kamishna huyo amewaasa washiriki wa warsha hiyo kutekeleza jukumu hilo  kwa uadilifu na uaminifu mkubwa ili kuziba mianya yote ambayo wahalifu wanaweza kuitumia kutimiza kusudi lao ovu na kuhatarisha usalama wa nchi.

 

Yanga kupimana ubavu na Ruvu Shooting
Wachezesha kamali wabanwa, sasa kuanza kulipa kodi TRA