Serikali imesema itaendelea kuwajengea uwezo wanawake ili kuweza kushiriki katika shughuli za matengenezo na ukarabati wa  miundombinu ya barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Mwanza (Tanroads) Eng. Marwa  Rubirya wakati akifungua mafunzo ya kozi kwa wanawake wa vikundi vya mikoa ya Kanda ya ziwa jijini Mwanza.

“Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya (Ujenzi) imekuwa ikitekekeza sera mbalimbali ikiwemo shughuli za matengenezo yenye kuongeza ushiriki wa wanawake katika kazi za barabara ili waweze kujikwamua kiuchumi”. amesema Eng.Rubirya.

Aidha, Rubirya amewataka  wanawake kusajili vikundi vyao kupitia bodi ya usajili wa Makandarasi nchini (CRB)  ili zabuni za kazi za ukarabati na matengenezo ya barabara zinapotangazwa waweze kukidhi vigezo vya kupata kazi hizo.

Vile vile, amewahimiza wakinamama hao kufanya kazi hizo kwa ubora unaotakiwa pindi wapatapo kazi hizo ili barabara hizo ziweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta faida kwa wananchi.

Kwa upande wake, muwezeshaji katika mafunzo hayo Eng. Liberata Alphonce amesema Serikali imelenga kuinua uchumi wa wanawake wenye nia ya kufanya kazi za barabara  kwa vile uchumi wa mwanamke ukiimarika na taifa pia litaimarika.

Naye Mratibu wa kitengo cha ushirikishaji wanawake katika kazi za barabara Eng. Rehema Myeya amesema Wizara imeona umuhimu wa kutoa mafunzo yatakayowasaidia wanawake kuwa na uwezo wa kufanya kazi za ukandarasi hasa wa barabara hususan matengenezo na ukarabati.

Hata hivyo, Teknolojia stahiki ya nguvu kazi inahusisha utumiaji wa rasilimali zilizopo pamoja na kutumia vitendea kazi rahisi na mitambo midogo midogo katika ujenzi na ukarabati wa barabara

Video: Makamba kuendesha operesheni tokomeza pombe kali aina ya Viroba
Nape awataka wadau wa michezo kushirikiana na Serikali