Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa lengo la kuwasaidia wakulima wapate mitaji ili waongeze tija.

Pia amewataka wakuu wa wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro wahahakikishe wanawahamasisha wananchi katika maeneo yao kuchangamkia fursa ya kilimo cha Miwa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo alipotembelea shamba la Miwa la Mkulazi na Mbigiri mkoani Morogoro alipokuwa njiani kwenda jijini Dodoma.

Amesema kuwa kuanzishwa shamba la Mkulazi ni katika jitihada za Serikali za kuhakikisha mahitaji ya sukari nchini yanafikikia katika kiwango kinachohitajika.

Majaliwa amesema kuwa Serikali imepanga kuzalisha sukari itakayotosheleza mahitaji na njia pekee  ni kuboresha kilimo cha miwa, kujenga viwanda vitakavyozalisha sukari ya kutosha.

Aidha, Majaliwa amemuagiza Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike apeleke wataalamu wengi wa kilimo katika shamba hilo ili wasaidie kusimamia kitaalamu.

“Nataka shamba hili lisimamiwe kitaalamu, uzalishaji uwe wa kitaalamu na liwe mfano na mashamba mengine, tusishindwe na watu binafsi,” amesema

Hata hivyo, ameongeza kuwa suala la maji hususan kipindi cha mvua ambayo huaribu shamba, Waziri Mkuu aliwataka watafute namna nzuri ya kuyahifadhi ili wayatumie kipindi cha kiangazi.