Serikali imesema kuwa bado inaendelea kuweka mikakati mizuri ya kuongeza usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) hapa nchini kwa kutegemeana na upatikanaji wa fedha.

Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe alipokuwa akijibu swali la mbunge, Zaynab Matitu Vulli (Viti Maalum) aliyeuliza Ni chanagamoto zipi zinazopelekea TBC kutosikika katika baadhi ya maeneo ya Pwani.

“TBC ina mitambo ya kurushia matangazo ya redio ya masafa ya FM katika Wilaya ya Kisarawe ambayo hufikisha matangazo kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani katika masafa ya  87.8 MHz kwa idhaa ya TBC Taifa, 90.0 MHzkwa idhaa ya TBC FM na 95.3 kwa idhaa ya TBC International”.Amesema Dkt. Mwakyembe.

Aidha ameongeza kuwa katika Bajeti ya mwaka 2016/17 TBC ilitekeleza mradi wa upanuzi wa usikivu katika Wilaya tano zilizopo mpakani ambazo ni Wilaya za Longido, Rombo,Tarime,Nyasa na Kibondo.

Vilevile katika Bajeti ya mwaka 2017/18 mradi wa usikivu katika mkoa wa Mtwara na Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ulitekelezwa ambapo hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu TBC ilikua na vituo thelathini na tatu vya kurushia matangazo katika masafa ya FM kwenye Wilaya 102 kati ya 161 nchi nzima.

Hata hivyo, Dkt. Mwakyembe ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa TBC inapanua usikivu ambapo kwa mwaka huu wa fedha maeneo ya Unguja na Pemba,Simiyu,Njombe,Songwe,Lindi maeneo ya Nangurukuru  pamoja na Mkoa wa Morogoro maeneo ya Morogoro Vijijini,Bondwa na Mahenge yatafikiwa.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Novemba 8, 2018
Ali Kiba kudhamini Wasafi Festival, Diamond aridhia