Serikali imesema kuwa bado kuna changamoto zinazokabili utekelezaji wa serikali mtandao ambapo baadhi ya mifumo ya Tehama kuendelea kutowasiliana na kutobadilishana taarifa ndani ya taasisi na kati ya taasisi na taasisi.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na kaimu katibu mkuu Micky Kiliba wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha serikali mtandao.

Amesema kuwa kuna mafanikio mengi yaliyopatikana kupitia wakala wa serikali mtandao ikiwemo kufanyika kwa uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya Tehama kama vile mkongo wa Taifa, vituo vya kitaifa vya data na kutenga masafa ya intaneti ya Serikali.

Aidha, amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo lakini bado kuna changamoto ya urudufu wa mifumo ambapo kila taasisi inakuwa na juhudi za kipekee katika kusimika na kutumia mifumo na miundombinu ya Tehama ambayo ingeweza kutumiwa na taasisi zaidi ya moja.

“Baadhi ya sababu zilizochangia uwepo wa changamoto hizi ni pamoja na kutozingatia miongozo na kanuni za usimamizi wa serikali mtandao zilizopo, upungufu wa wataalamu wa Tehama wenye uwezo na ujuzi wa kutosha, misukumo kutoka kwa wafanyabiashara na wafadhili na uratibu hafifu wa shughuli za Tehama ndani na kati ya taasisi za serikali,” amesema Dkt. Ndumbaro.

Kwa upande wake Kaimu katibu Mkuu, Micky Kiliba amewataka Watumishi wa umma kuutambulisha mfumo huo kwa serikali mtandao kwa wananchi ili kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma.

“Hata katika masuala ya uwekezaji hakutakuwa na haja ya wawekezaji kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kupata taarifa za uwekezaji watakuwa wanaingia kwenye mfumo wetu na kujua kila kitu
wanachokihitaji bila hata ya kuja huku,” amesema Kiliba

Mahakama yamfungia mipaka na benki mpinzani wa Maduro
Aliyefanyiwa vibaya oparesheni ya kichwa kulipwa bilioni 1

Comments

comments