Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu maelezo yanayotolewa na baadhi ya watu juu ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa Mwaka 2016, kuhusu utambuzi wa elimu ya mwandishi wa habari.

Akizungumza kupitia Hatua Tatu ya 100.5 Times Fm, Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo, Hassan Abbas amekanusha taarifa zinazodai kuwa kupitia mswada huo, mwandishi wa habari atakayekuwa anatambulika ni yule mwenye shahada ya masuala ya uandishi wa habari tu.

“Hakuna sehemu yoyote kwenye muswada huu ambayo inasema mwandishi atakuwa ni mwenye shahada, hili limeachwa liwekwe kwenye kanuni kutokana na changamoto ya uwekaji wa viwango vya elimu kwenye tasnia hii kwa ujumla,” alisema Abbas.

Alifafanua kuwa kwa kuwekwa kwenye kanuni, ni rahisi baadae kufanya mabadiliko kadri inavyowezekana kwani anayesaini Kanuni ni Waziri mwenye dhamana lakini kubadili kipengele chochote kwenye sheria ni lazima kuirudisha Bungeni.

“Hili lilikuwa changamoto kubwa hata kwa wajumbe wa kamati ya Bunge ambao walikaa siku tatu kujadili kipengele hiki cha kiwango cha elimu cha kumtambua mwandishi lakini walishindwa kupata jibu la moja kwa moja,” alieleza.

Msemaji huyo wa Serikali alisema kuwa changamoto kubwa katika upangaji wa kiwango cha elimu ni kuwa wapo baadhi ya watu wanaofanya kazi ya kupitia maandishi (proof reading), kupiga picha tu na kazi nyingine za kawaida ambazo ni vigumu kuweka moja kwa moja kiwango cha shahada kuwapima.

Ametoa wito kwa waandishi wa habari wote pamoja na wadau kuusoma mswada huo ili kuepuka upotoshwaji.

Muswada huo wa habari unaelekeza mwandishi wa habari kuwa na kiwango cha elimu kinachotosheleza lakini haikuweka wazi kiwango hicho.

Video: Mchambuzi wa Michezo afunguka ya chini ya kapeti Simba, Yanga kutaka kubadili mifumo
Meya wa CCM mbaroni kwa kuisababishia Serikali hasara ya Shilingi Milioni 226