Tume ya Kimataifa ya wataalamu wa Haki za binadamu, imezitaka Serikali ya Ethiopia na chama cha Tigray People’s Liberation Front, kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwani kutokuelewana kwao kunasababisha mateso kwa raia.

Taarifa iliyotolewa na wataalamu hao wa Haki za binadamu kutoka jijini Geneva nchini Uswisi imesema, mapigano hayo yanazidisha ugumu wa maisha kwa raia katika eneo hilo la Tigray na kuna hatari kubwa ya kuongezeka kwa vifo, majeruhi na hali ngumu ya maisha.

Wamesema, “Tuna wasiwasi hasa kuhusu ripoti za vifo vya raia katika uwanja wa michezo huko Mekelle katika eneo la Tigray, na madai ya kuwalenga raia katika mashambulizi mapya huko Kobo katika eneo la Amhara.”

Wataalamu hao, wametoa wito kwa wahusika kusitisha mapigano mara moja na kurejea katika mchakato wa mazungumzo ambao kila mmoja ataukubali ili kuondoa sintofahamu baina yao na kuleta amani.

“Tunazihimiza zaidi pande zote mbili kuchukua mara moja hatua zote zinazohitajika ili kuruhusu Umoja wa Mataifa na mashirika mengine kutekeleza usambazaji wa misaada ya kibinadamu huko Tigray,” imesema taarifa hiyo.

Hata hivyo, taarifa hiyo imehitimisha kwa kusema haki za binadamu, afya, na ustawi wa raia lazima ziwe kipaumbele cha juu kwa pande zote na kwamba kupigana kwa kuangalia maslahi yao kunadhuru watu wasio na hatia kitu ambacho hakifai.

Wataalamu kutathmini athari kinu cha Nyuklia
Tamasha 'International Afrika Epo Festival' kufanyika Ujerumani