Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imepiga marufuku mikutano yote ya kisiasa kwenye mji mkuu Kinshasa kwa wagombea wote wa urais siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa kihistoria kufanyika nchini humo.

Gavana wa jiji la Kinshasa, Andre Kimpita, amesema kuwa hatua hiyo ya kupiga marufuku mikutano ya siasa imechukuliwa kwa sababu za kiusalama hasa wakati huu nchi inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Tangazo hilo ambalo halikutarajiwa limekuja wakati mgombea mkuu wa upinzani, Martin Fayulu alikuwa azindue kampeni yake ya kisiasa jijini Kinshasa.

Aidha, uchaguzi huo mkuu ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 23 mwezi huu wa kumtafua mrithi wa Rais, Joseph Kabila umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara na itakuwa ndiyo mara ya kwanza kutakuwa na mabadiliko ya uongozi kwa njia ya amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hata hivyo, chama tawala nchini DRC kimemteua, Emmanuel Ramazani Shadary waziri wa zamani wa mashauri ya ndani na mwaminifu kwa Rais Joseph Kabila kuwa mgombea wake.

Video: Magufuli afuta ndoto za fidia, Bodi ya mikopo yakusanya bil. 15 kwa mwezi
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 20, 2018