Serikali ya Kenya imesema kuwa wasafiri watakaoingia nchini humo kutoka Tanzania hawatarudishwa kwani nchi hizo zimeshaweka sawa sintofahamu iliyojitokeza hivi karibuni.

Waziri wa Uchukuzi wa Kenya, James Macharia amesema kuwa ingawa Tanzania haikuwa kwenye orodha ya nchi 19 ambazo ndege zake zimeruhusiwa kutua nchini humo, haimaanishi kuwa imezuiwa.

“Wasafiri kutoka Tanzania wanaweza kuingia kuanzia leo [Agosti 1, 2020]. Hatujazuia ndege za Tanzania. Hili ni suala dogo na tayari tumeshalimaliza na tunaamini kama sio leo basi kuanzia kesho mtaona ndege za Kenya zikisafiri kwenda Tanzania,” amesema Macharia.

Waziri Macharia alifafanua kuwa orodha ya ndege za nchi zilizoruhusiwa haimaanishi kuwa zile zote ambazo haziko kwenye orodha hazijaruhusiwa kufanya safari zake nchini humo.

“Haitakuwa sawa kuanza kujadili nchi moja moja kwa sababu tuna jumla ya nchi 180 lakini hadi sasa ni nchi 19 tu ambazo ziko kwenye ile orodha ya kuingia Kenya bila masharti ya wasafiri kuwekwa karantini,” amesema.

Mamlaka ya Anga ya Tanzania ilitoa barua iliyoeleza kuzuia ndege za Kenya kutua nchini, baada ya kuona taarifa ya orodha ya ndege za nchi zilizoruhusiwa kufanya kazi zake nchini humo ambapo Tanzania haikuwa miongoni.

Aidha, Waziri Macharia aliongeza kuwa shughuli zinaendelea kama kawaida katika mipaka ya Namanga na Malaba, watu wanavuka kati ya nchi hizo mbili.

Hata hivyo, alisema kuwa wameweka utaratibu ambao hivi sasa utakuwa ni siri hasa kwa usafiri wa anga, kwa lengo la kuendelea kujikinga dhidi ya virusi vya corona.

Ndege za Kenya zapigwa ”stop” Tanzania

Spurs, Arsenal zabanana kwa Coutinho

Gavana Kenya apinga ripoti ya Wizara, adai hakuna Covid-19 kwake
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Agosti 2, 2020