Serikali ya Uganda imeonesha nia ya kumpa hifadhi aliyekuwa Rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir, ambaye Baraza la Usalama la Kijeshi limemuweka kwenye jela yenye ulinzi mkali.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Okello Oryem amesema kuwa Rais Yoweri Museveni anaweza kufikiria kumpa hifadhi al-Bashir endapo ataomba.

“Kama Omar al-Bashir ataomba hifadhi hapa Uganda ni suala ambalo linaweza kufikiriwa na Rais wa Uganda,” Oryem amesema.

Oryem amemuelezea al-Bashir akimuita Rais, kuwa alifaa kupewa heshima kutokana na mchango wake katika kuitafuta amani Sudan Kusini.

“Rais Omar Bashir alikuwa kinara wa makubaliano ya amani ya Sudan Kusini, alifanya kazi kubwa na muhimu ambayo tunaiheshimu na kumshukuru, kwahiyo hifadhi kwa Uganda ni suala ambalo linaweza kufikiriwa,” Waziri huyo aliwaambia waandishi wa habari.

Utawala miaka 30 wa a-Bashir ulifikia ukingoni wiki kadhaa zilizopita kufuatia maandamano ya wiki 16 mfululizo nchini humo yaliyolenga kumuondoa madarakani.

Baraza la Ulinzi la Jeshi ndilo linaloiongoza Sudan, huku kukiwa na shinikizo kubwa kutoka kwa waandamanaji kulitaka kuunda Serikali ya kiraia haraka iwezekanavyo.

Rais Magufuli atoa wiki moja kwa Wizara ya Ardhi, Wizara ya Viwanda kumpatia mwekezaji eneo
Mkate wageuka anasa Zimbabwe, bei yapaa