Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameiagiza Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) kuhakikisha inaandaa mkakati na mapendekezo kwa serikali namna ya kuthibiti ushiriki wa Watoto chini ya miaka 18 kujihusisha na michezo hiyo.

Ametoa agizo hilo Jijini Dar es Salaam alipotembelea na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Bodi hiyo pamoja na wafanyakazi, katika mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.

“Katika eneo hili ya ushiriki wa Watoto katika michezo ya kubahatisha niseme kwamba kama wasimamizi mliopewa jukumu la kudhibiti Watoto kushiriki michezo hiyo hamjafanya kwa viwango vya kutosha na sijaona maelezo ya kimkakati ya kuridhisha”, Amesema Mhandisi Masauni.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), James Mbalwe amehaidi kulifanyia kazi suala la watoto chini 18 kutokushiriki michezo hiyo ili kujenga jamii bora kwa manufaa ya baadae ya maendeleo na ustawi wa Taifa.

Amesema kuwa Michezo ya kubahatisha nchini imeajiri zaidi ya watu 20,000 kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021, michezo hiyo imewezesha kuwepo kwa mzunguko wa fedha katika sekta ya michezo ya kubahatisha unaofikia zaidi ya shilingi trilioni 3.2 na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Taasisi ya GBT inachangia Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo mwaka 2020/2021 walichangia shilingi bilioni 3.05 na kwamba azma ya GBT ni kuendelea kuchangia katika mfuko huo kwa mujibu wa Sheria na miongozo inayotolewa na Serikali.

Rais Samia kupokea ndege mpya ya 9 kesho
Rais Mwinyi 'sera ya mambo ya nje izingatie faida za pande zote za Muungano'