Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amefungua mkutano wa kitaalamu wa African Minerals Geosciences Initiative (AMGI), wa kuainisha maeneo ya kipaumbele sambamba na mkakati wa Serikali kuboresha taarifa za Jiosayansi ya uwekezaji Sekta ya Madini ukiwajumuisha wawekezaji toka Korea ya Kusini.

Mkutano huo umefanyika jijini Dar es Salaam Agosti 30, 2022 ukilenga kufunga awamu ya kwanza ya utafiti wa Jiosayansi katika nchi tatu za Afrika za Tanzania, Zambia na Msumbiji, ambapo Dkt. Kiruswa amewahakikishia wawekezaji kuwa Serikali itatoa ushirikiano wa mazingira ya utafiti.

Amesema, anatambua Korea Kusini ni miongoni mwa nchi zilizoendelea kiteknolojia duniani, na hivyo kupelekea uhitaji mkubwa wa madini ya teknolojia kama vile kinywe, nikeli, niobium na REE.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dkt. Mussa Budeba aliishukuru Serikali ya Korea Kusini na Umoja wa Mataifa ya Afrika, kwa kuamua kufanya mkutano huo nchini Tanzania na kuahidi kushirikiana kufanya tafiti kwenye maeneo ya nchi.

Akiahirisha mkutano huo wa siku mbili kwa siku ya kwanza, Kamishna wa Madini Tanzania Dkt. Abdulraham Mwanga aliwashukuru washiriki na kuwakumbusha umuhimu wa madini katika maisha ya sasa hivyo, na kusema Bara la Afrika linatakiwa kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza rasimali madini.

Utafiti wa Jiosayansi umefanyika katika maeneo ya Tunduma Mkoani Songwe na sehemu za Wilaya za Tunduru, Namtumbo na Songea Mkoani Ruvuma chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa ya Afrika na kudhaminiwa na Serikali ya Korea Kusini.

Mkutano huo umehudhuliwa na washiriki wa mradi wa AMGI kutoka nchi jirani za Zambia na Msumbiji, wawakilishi kutoka GST, Wizara ya Nyumba, Ardhi na Makazi Tanzania, Idara ya Upimaji na Ramani, ujumbe kutoka Korea Kusini, Mkurugenzi Msaidizi ofisi ya Kamishina wa Umoja wa Mataifa na wawakilishi kutoka kituo cha Madini na Jiosayansi cha Afrika (AMGC).

Marekani yasimama 'Made in Lagos' ya Wizkid
KMC FC yaitangazia vita Simba SC