Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, amesema kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha wakulima wa zao la mwani kwa vifaa pamoja na utaalamu ili waweze kuzalisha kwa wingi na ubora unaohitajika sokoni.

Ameyasema hayo katika Kijiji cha Zingibari kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, wakati akitoa vifaa vyenye thamani ya Shilingi Milioni Nne kwa ajili ya kilimo cha mwani kwa vikundi vitatu vya wakulima wa zao hilo, huku kufafanua kuwa serikali itaendelea kutoa bure vifaa hivyo kwa wakulima wa mwani katika mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi ili kuhakikisha zao hilo linalimwa kwa wingi nchini.

Akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Tanga, Waziri Ndaki amesema kutokana na zao la mwani kuwa la kiuchumi kwa wananchi wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi, serikali imeanza kuweka mazingira mazuri ya uwezeshaji na kutafuta masoko ya uhakika ili wakulima waweze kunufaika kiuchumi.

Hali kadhalika Waziri Ndaki, amesema serikali inatarajia kutumia Shilingi Bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kimataifa katika kata ya Kipumbwi Wilaya ya Pangani mkoani Tanga kwa ajili ya kuuza dagaa ndani na nje ya nchi.

Kuhusiana na uvuvi haramu Waziri Ndaki, amesema serikali itavunja Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) ambavyo vitabainika kujihusisha na uvuvi haramu na kuhakikisha viongozi wa vikundi hivyo wanafikishwa Katika vyombo vya sheria.

“Baadhi ya BMU zimeshindwa kutekeleza wajibu wake na kushirikiana na wavuvi haramu acheni mara moja kabla hamjakumbana na mkono wa sheria, yeyote atakayematwa anajihusisha na uvuvi haramu atachukuliwa hatua kali za kisheria.” Amesema Waziri Ndaki.

Katika sekta ya mifugo, Waziri Ndaki pia ametembelea mnada wa mpakani wa Horohoro kujionea miundombinu mbalimbali inayowekwa kabla ya kuanza rasmi kwa mnada huo ambao anasema utakuwa na matokeo chanya pindi utakapokamilika.

“Licha ya kusaidia kupunguza utoroshaji wa mifugo mnada utasaidia kuongeza kipato kwa wananchi na hivyo kuinua uchumi wao, kwa sababu wakipeleka ng’ombe nje ya nchi wanauza bei ya juu lakini pia tunataka tuwapunguzie wananchi adha ya kuvuka mipaka kwani jambo hili wakati mwingine linasababisha kuuza mifugo yao kwa bei ya chini.” Amesema Waziri Ndaki.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki akizungumza na wakazi wa Kata ya Kipumbwi iliyopo Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo na kusisitiza kuwa serikali inatarajia kujenga soko la kimataifa la samaki aina ya dagaa katika kata hiyo na kutoa onyo kwa watu wanaohusika na uvuvi haramu nchini kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na wakazi wa Kata ya Kipumbwi iliyopo Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga, na kuwafahamisha mikakati ya serikali katika kuhakikisha sekta ya uvuvi inawanufaisha wananchi ikiwemo ya kufanya marekebisho ya sheria na tozo mbalimbali, wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki Mkoani Tanga.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki akimkabidhi mmoja wa wanachama wa vikundi vya wakulima wa zao la mwani katika Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, vifaa vya kulimia zao hilo zikiwemo kamba na kufafanua kuwa serikali itahakikisha misaada ya vifaa vya namna hiyo itasambazwa maeneo mbalimbali nchini katika mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi panapolimwa zao la mwani ili kukuza zao hilo na kuliongezea thamani.

TBC kutangaza Ligi Kuu miaka kumi
Naibu Waziri Kundo akukagua muingiliano wa mawasiliano mipakani