Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imekusudia kufanya msako mkali kwa wafanyakazi wasio raia wa Tanzania wanaofanya kazi nchini kinyume cha sheria na taratibu ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa ndani (house girls/boys).

Operesheni hiyo itakayowagusa hadi wafanyakazi wa ndani ni sehemu ya ile iliyoanzishwa na wizara hiyo ambayo tayari imeshawatia nguvuni watu 79 waliobainika kufanya kazi nchini bila kuwa na vibali kuanzia wiki kadhaa zilizopita.

Msemaji wa wizara hiyo, Isaac Nantanga aliwataka wale wote waliowaajiri raia wa kigeni kinyume cha sheria kuwaondoa kazini mara moja kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria. Aliongeza kuwa serikali haijakurupuka kama baadhi ya watu wanavyodai na kwamba zoezi hilo linaenda kwa kasi na ufanisi.

“Nawatahadharisha wale wote wanaodai kuwa tumekurupuka, watambue kuwa hakuna mgeni yeyote anayeruhusiwa kufanya kazi nchini kinyume cha Sheria, hivyo wale wote wanaoendelea kuwaajiri wageni wa aina hiyo wamevunja Sheria,”Nantanga anakaririwa.

Aliwataka wananchi kushirikiana na idara ya uhamiaji kutoa taarifa zitakazowezesha kuwabaini raia wa kigeni wanaofanya kazi kinyume cha sheria nchini huku akisisitiza kuwa hakuna raia wa kigeni asiye na kibali atakayebaki.

Washindi wa Tuzo za Golden Globes 2016 wako hapa
Mkwasa Amkabidhi Kitambaa Cha Taifa Stars Samatta