Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imebaini kuwa maeneo ya bahari kuu, bandari, vituo vya mabasi na viwanja vya ndege yanatumika sana katika kupitisha dawa za kulevya.

Amesema kuwa wafanyabiashara, wasambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya wameendelea kukamatwa, lengo ni kuhakikisha biashara hiyo inamalizika nchini.

Ameyasema hayo hii leo jijini Dar es salaam wakati akikabidhi gari kwa Kamishna Generali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga.

Aidha, amesema mbali na kukamata meli, pia Serikali imewakamata wasambazaji pamoja na kundi kubwa la wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya sambamba na watumiaji, lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na kizazi chenye uwezo wa kuzalisha mali.

Vile vile ameongeza kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya dawa za kulenya, ambapo hivi karibuni imekamata meli nyingi, moja ilikiwa inatokea pwani ya Msumbiji na ilikamatiwa maeneo ya Mtwara ikiwa na dawa nyingi za kulevya.

“Niwakati wa Serikali kuendelea kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na leo hii tunawakabidhi gari hili jipya kabisa ili iweze kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake ipasavyo.”amesema Majaliwa

 

Kwa upande wake Sianga ameishukuru Serikali kwa kuipatia mamlaka hiyo gari, ambapo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi waachane na biashara ya dawa za kulevya. Alisema wanapambana kuhakikisha dawa za kulevya ili zisiingie nchini.

 

Dkt. Tulia adai hoja ya Peneza haikufuata utaratibu
TRA yakamata madumu 500 ya mafuta kwa kukwepa kodi