Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya (DCEA), imebaini mbinu mpya za wafanyabiashara wa dawa za kulevya waliounda aina mpya ya dawa hizo na kubadili mfumo wa uwasilishaji.

Kamishna Msaidizi wa DCEA, Ziliwa Machibya amesema kuwa wafanyabiashara hao wamegundua na kutengeneza dawa za aina nyingine tofauti kabisa na heroine au cocaine, lakini zenye athari sawa na dawa hizo na kisha kuziweka kwenye mfumo wa vidonge na pipi.

Machibya alisema kuwa aina hiyo mpya ya dawa za kulevya zinazoitwa New Cycle Active Substances, inawalenga zaidi wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

“Mtu akiwa na kemikali bashirifu, anaweza kutengeneza dawa hizi akiwa nyumbani na kuingiza sokoni na zinaweza kuwa katika mfumo wa pipi, vidonge, unga au mfumo wowote ili mtumiaji azitumie, lengo likiwa kukwepa mkono wa sheria,” Machibya aliiambia Mwananchi.

“Hizi dawa mpya zina athari katika mfumo wa fahamu. Jinsi mfumo wa fahamu unavyoathirika ni sawa ambavyo mtu angetumia dawa nyingine,” aliongeza.

Amesema kuwa wamejipanga kuanzisha msako maalum kuwakamata wahusika pamoja na kubaini kiwango cha dawa hizo kilichoingia sokoni na chanzo chake.

DCEA wakishirikiana na taasisi nyingine zisizo za kiserikali, wamefanya kampeni kwenye shule kadhaa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwaelimisha wanafunzi athari za dawa hizo, kwa lengo la kuwaepusha.

Nicki Minaj, Young Money wazitosa tuzo za BET, Sifa kwa Cardi B zachochea
Mpinzani DRC aandika barua nzito kutaka uchaguzi urudiwe