Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu imewataka wananchi kupuuza kile ilichoeleza kuwa ni upotoshaji kuhusu hatua ilizochukua kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge, Uledi Mussa, imeeleza kuwa tayari ilishachukua hatua za awali ikiwa ni pamoja na kuwagharamia matibabu majeruhi wote 560, kugharamia mazishi ya watu 17 pamoja na kutoa mkono wa pole wa shilingi milioni 1.8 kwa wafiwa.

Taarifa hiyo ya Serikali imekuja wakati ambapo kumekuwa na sintofahamu baada ya serikali ya Mkoa wa Kagera kueleza kuwa kiasi cha fedha kilichopatikana kupitia akaunti maalum ya kuchangia, kitaelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya umma na kuwataka wananchi kujenga nyumba zao wenyewe.

Mussa kupitia taarifa yake amesema kuwa tathmini ya kitaalam iliyotolewa imeonesha kuwa kiasi cha shilingi bilioni 104.9 ndicho kinachohitajika ili kurejesha hali ya awali ya mkoa huo.

Aliongeza kuwa kiasi cha shilingi bilioni 1.92 ni kwa ajili ya kugharamia kodi ya nyumba ya miezi sita kwa waathirika ambao hawana makazi na wamelazimika kupanga sehemu nyingine. Ukarabati wa jumla ya shule 210 utagharimu takribani shilingi bilioni 58.

Kadhalika, vituo vya afya na zahanati 32 zitagharimu shilingi milioni 772 na majengo ya taasisi 20 utakaogharimu shilingi bilioni 1.3.

Katika hatua nyingine, wabunge wa mkoa huo wa CCM na wale wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa wamepanga kufanya vikao vya dharura kujadili hali ya utoaji wa misaada katika eneo hilo.

“Tunajiandaa na kikao ambacho ni cha dharura. Wabunge wote wa Kagera tutajadili suala hili maana (suala) hili lilitokea wakati tukiwa Bungeni na hatukupata muda wa kujadili kwa sababu kulikuwa na misiba,” Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CCM), Rwegasira Mukasa anakaririwa na Nipashe.

Kwa upande wake Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema) alisema kuwa kitendo cha Serikali kuelekeza fedha hizo kwa ukarabati wa miundombimu kunaonesha ni jinsi gani haijajipanga katika mfuko wa maafa.

Wabunge hao walieleza kuwa hawakuridhishwa na uamuzi wa Serikali kuelekeza fedha zote kwa ujenzi wa miundombinu ya umma kwani walitarajia wananchi walioathirika wangepewa kipaumbele kwanza.

Gareth Southgate: Nimeleta Mabadiliko Kikosini
Lowassa aeleza kwanini hakuhudhuria misiba ya Sitta, Mungai