Serikali imefuta mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira 36 ambazo sasa zitahudumiwa na mamlaka za makao makuu ya mikoa zilizoundwa na kuongezewa majukumu ya utoaji huduma katika maeneo yake kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza matumizi ya fedha

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Prof. Kitila Mkumbo ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya Wizara juu ya maboresho ya muundo mpya wa mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira nchini.

Amesema baadhi ya mamlaka za maji na usafi wa mazingira zilizofutwa kati ya 36 ni pamoja na Kibaha WSSA, Kongwa WSSA, Chamwino WSSA, Kilosa, Kyela WSSA, Mikumi WSSA, Pangani WSSA na Magugu WSSA.

Prof. Mkumbo ameongeza kuwa katika kuimarisha uendesahiji wa sekta ya usambazaji maji na usafi wa mazingira mijini Waziri wa maji Profesa Makame Mbarawa kwa mamalaka aliyonayo kisheria ameongeza maeneo ya huduma za maji.

“Kwa kutumia sheria ya huduma za maji na usafi wa mazingira namba tano ya mwaka 2019 Waziri ameongeza maeneo ya huduma kwa baaadhi ya mamalaka za maji na usafi wa mazingira na ameanzisha na kufuta baadhi ya mamlaka za maji na usafi wa mazingira,” amefafanua Prof. Mkumbo

Ameongeza kuwa katika mabadiliko hayo kutakuwa na mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira 25 katika ngazi ya makao makuu au miji mikuu ya mikoa na kwamba zitahudumia halmashauri zilizopo katika miji mikuu, na makao makuu ya mikoa.

“Baadhi ya mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira katika ngazi hii zimeongezewa maeneo ya huduma na kuunganishwa na baadhi ya miji midogo katika mikoa husika au mikoa ya jirani hivyo utaratibu unakuwa rasmi kisheria,” amesema Profesa huyo.

Aidha Prof. Mkumbo amezitaja baadhi ya mamlaka za maji na usafi wa mazingira za mikoa zilizoongezewa majukumu kuwa ni mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Dar es saalam (DAWASA) ambayo itahudumia hadi maeneo ya Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe na Mkuranga.

Nyingine ni mamlaka ya maji na usafi wa mazingira mkoa wa Dodoma (DUWASA), ambayo itahudumia eneo la jiji na miji ya Kongwa, Bahi na Chamwino na mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Mrogoro (MORUWASA) ambayo imeongezewa miji ya Kilosa na Mikumi.

Amesema nyingine ni Mamalaka ya maji na usafi wa mazingira ya Mwanza (MWAUWASA) ambayo itahudumia halmashauri ya jiji la Mwanza, manispaa zake na mji wa Magu, Nansio na Ngudu na kwamba miji midogo ya wilaya 40 zitasimamiwa na mamlaka ya maji vijijini (RUWASA).

LIVE: Rais Magufuli akizindua kitabu cha Mkapa ''My Life, My Purpose''
Mfumuko wa bei wa Taifa wapanda