Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni tano kwa ajili  ya ujenzi wa studio za Redio na Runinga za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) katika makao makuu ya nchi Dodoma.

Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Antony Mavunde alipokua akijibu swali la Anna Richard Lupembe mbunge wa Viti Maalum aliyeuliza kuwa ni lini Redio Tanzania (TBC Taifa) itasikika katika kata za Ilela na Ilunde Wilayani Mlele.

Mavunde ambaye amejibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kupanua usikivu wa TBC katika Mikoa na Wilaya ambazo  hazina usikivu au kuwa na usikivu hafifu ambapo katika bajeti ya mwaka2018/19 kiasi cha shilingi Bilioni moja zilitengwa kwa ajili ya kupanua usikivu katika wilaya tano za mpakani mwa nchi.

“Mkakati wa Serikali ni  kujenga mitambo ya redio katika mikoa ya Songwe, Katavi, Njombe na Simiyu katika bajeti ya mwaka 2019/20  na katika bajeti ya mwaka 2018/19 TBC imetengewa kiasi cha shilingi Bilioni tano kwa ajili ya kujenga studio za redio na luninga makao makuu ya nchi Dodoma”. Alisema Mhe. Mavunde.

Hata hivyo, Mavunde ameongeza kuwa maeneo ambayo mitambo imefungwa na tayari  matangazo ya redio yamewashwa ni Rombo, Nyasa (Mbambabay), Tarime, Kibondo/Kakonko na Namanga kwa ajili ya kuongeza usikivu wa TBC.

Video: Kifo humkuta mtu sehemu yoyote - Lugola
Watendaji wa Serikali wapigwa marufuku kusimamia uchaguzi