Serikali imekamilisha upanuzi wa Chuo cha Ualimu Patandi ili kukiongezea uwezo wa kudahili walimu wenye taaluma ya elimu maalum wanaohitajika nchini ili kupunguza changamoto ya walimu hao.

Hayo yamesemwa bungeni Jijini Dodoma na Mhandisi, Stella Manyanya alipokuwa akijibu swali la Grace Victor Tendega Mbunge wa Viti Maalum kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako juu ya mpango wa Serikali katika kuhakikisha walimu wenye weledi wa watu wenye ulemavu wanatosheleza nchini.

“Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu wenye Taaluma ya Elimu Maalum, Changamoto hii inasababishwa na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wenye ulemavu kutokana na mabadiliko chanya ya kimtazamo na uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watu wenye ulemavu,” amesema Mhandisi Manyanya.

Aidha, amesema kusema, mahitaji ya walimu wa elimu maalum nchini ni walimu 8,882 katika shule maalum na vitengo vinavyopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum 706, ambapo hadi kufikia Disemba 2018 walimu 5,556 wenye Taaluma ya Elimu Maalum ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada walihitimu katika vyuo mbalimbali nchini vikiwemo Chuo cha Ualimu Patandi na Chuo  Kikuu Dodoma.

Hata hivyo, ameongeza kuwa hatua ya Serikali ya kuanzisha kozi ya elimu maalum katika ngazi ya Astashahada Chuo cha Ualimu Patandi kwa walimu tayari kwa mwaka wa masomo 2018/19 itaongeza idadi wa walimu wanaojiunga na mafunzo ya Ualimu wa Elimu Maalum ili kupunguza changamoto ya walimu wenye elimu hiyo wanaohitajika nchini.

 

Masele afunguka baada ya kuhojiwa na Kamati ya Bunge
Video: Stonebwoy ahatarisha maisha ya Shatta Wale