Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni imesema kuwa hakuna Sheria yeyote inayomruhusu Askari Polisi kumpiga au kumtesa mtuhumiwa wa makosa mbalimbali kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya Askari kufanya vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na sheria ya nchi.

Hayo yamezungumzwa leo Bungeni jijini Dodoma ambapo amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya mienendo ya makosa ya jinai kifungu cha 11 kimeeleza namna ya ukamataji na imekataza unyanyasaji wa aina yeyote kwa raia au watuhumiwa waliopo mikononi mwa polisi.

Ameongezea kuwa askari atakayekutwa na makosa hayo hatua za kinidhamu zitachukuliwa ambapo anaweza kufukuzwa kazi au kupelekwa mahakamani.

”Askari polisi kabla hajaajiliwa wanapewa mafunzo ya namna ya kufuata sheria na kanuni hizo, hayo ni matatizo ya askari mmoja mmoja na tunapogundua askari anafanya vitendo vya kuwanyanyasa raia huwa tunamchukulia hatua” amesema Masauni.

Aidha, ametoa wito kwa raia kutoa taarifa mahali husika kwa askari ambao watawanyanyasa bila kufuata kanuni na sheria za kazi zao.

 

Video: Serikali yatimiza ahadi yake kuhusu Familia ya marehemu Mzee Majuto
Serikali yatoa wito kwa wadau kukarabati kituo cha kitalii

Comments

comments