Wakati utoro kazini na uchelewaji ukitajwa kuwa moja kati ya majipu yaliyo kwenye foleni ya kutumbuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, mfumo wa kisayansi wa kubaini mahudhurio kwa njia ya kielekroniki umetajwa kuwa mwarubaini.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa serikali inaendelea kufunga mfumo wa kielekroniki wa EAR kwa ofisi zote za umma ili kuhakikisha watumishi wa umma wanafika ofisini kwa wakati na kuwabaini watoro.

Profesa Mbarawa aliyasema hayo muda mfupi baada ya kujisajili kwenye mfumo huo uliofungwa katika ofisi ya Wizara yake jijini Dar es Salaam ambapo aliutaka uongozi kuhakikisha kila mtumishi anatumia mfumo huo.

“Hakikisheni watumishi wote wanatumia mfumo huu wa kieletroniki ili kudhibiti utoro na kuhakikisha watu wanafanya kazi kwa muda unaokubalika kiserikali,” alisema Profesa Mbarawa.

Alieleza kuwa mfumo huo utakapofungwa katika taasisi zote za umma utadhibiti watoro kwa kuwa unaweka kumbukumbu ya muda ambao mtumishi anakuwa kazini hivyo kuwezesha kufahamu taarifa sahihi za mahudhurio.

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kingwangalla aliwafungia geti watumishi wa wizara yake waliochelewa kazini baada ya muda wa kazi ambao ni saa 1:30 asubuhi. Kigwangalla aliahidi kupambana na watoro huku akikagua daftari la mahudhuri. Hivyo, uwepo wa mfumo wa kielekroniki utakuwa njia rahisi kwa viongozi kama Kigwangalla kuwashika watoro bila kuwavizia.

Lowassa ajifananisha na marais hawa, afuata nyayo za Maalim Seif
Maajabu ya Christmas: Taswira ya mtu akitembea juu ya mawingu yazua gumzo