Siku moja baada ya aliyekuwa naibu waziri wa Kazi na ajira, Dk. Makongoro Mahanga kukosoa uteuzi wa makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu kwa madai kuwa idadi yao inakinzana na dhana ya kupunguza matumizi na ukubwa wa serikali, serikali imeyatolea majibu.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue emeeleza kushangazwa na kauli hiyo ya Dk. Mahanga na kufafanua kuwa uteuzi huo wa makatibu wakuu hauna uhusiano na baraza la mawaziri kwani sio sehemu ya baraza hilo.

“Kwa mtu aliyekuwa naibu waziri kwa muda mrefu sana, inashangaza hajui kuwa makatibu wakuu si sehemu ya Baraza la Mawaziri. Idadi yao si kipimo cha ukubwa au udogo wa Baraza la Mawaziri,” alisema Balozi Sefue.

Balozi sefue aliongeza kuwa jumla ya idadi ya makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu walioteuliwa na rais John Magufuli hivi karibuni ni ndogo ukilinganisha na idadi ya serikali iliyopita.

“Jumla ya makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa Serikali iliyopita ilikuwa 54. Hivi sasa wako 49 tu,” alisema.

Awali, Dk. Mahanga ambaye alitangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema siku chache baada ya kushindwa katika zoezi la kura za maoni, alisema kuwa kuteua makatibu wakuu 27 ni sawa na kuwa na wizara 27 badala ya 15 kama inavyoelezwa kupitia mawaziri walioteuliwa. Alisema kuwa Katibu Mkuu ndiye mtendaji katika wizara na sio waziri, kwa kuwa ofisi ya wizara ni ya katibu mkuu.

 

Kubenea Azungumzia Tuhuma Za Wizi Wa Mali na Jina la Nduguye, Ukanjanja
Basi lauwa baada ya kugongana na Roli