Serikali kupitia wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imesema kuwa haikukurupuka kufanya manunuzi ya ndege mbili aina ya Bomberdier Q400 kutoka nchini Canada, bali ilizingatia uhalisia wa mazingira na mahitaji ya nchi.

Ufafanuzi huo wa serikali umekuja siku chache baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kukosoa uamuzi huo wa Serikali hususan aina ya ndege zilizonunuliwa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa ndege hizo ni bora kwa matumizi nchini kwani zina uwezo wa kutua katika viwanja vingi zaidi vya ndege nchini tofauti na zilivyo ndege nyingine hivi sasa.

“Serikali haikukurupuka katika kufanya maamuzi aina ya ndege za kununua badala yake imezingatia vigezo na malengo mahususi ya kuhudumia usafiri wa ndani na kuboresha usafiri wa anga kupitia shirika la ndege Tanzania (ATCL)”, alisema Profesa Mbarawa.

Kadhalika, Profesa Mbarawa amesema kuwa uendeshaji wa ndege hizo ni nafuu kwani hutumia kiasi kidogo cha mafuta kulinganisha na ndege nyingine. Alisema ndege hizo hutumia tani 1.7 kwa safari moja wakati ndege nyingine hutumia hadi tani 2.8 kwa safari kama hiyo.

Aliongeza kuwa sio kweli kama ndege hizo zimenunuliwa katika Kampuni ndogo isiyo na uzoefu kwani kampuni hiyo imeshaziuzia nchi kama Ethiopia na zimefanikiwa katika uendeshaji wa ndege hizo.

Ndege hizo zinatarajiwa kuingia nchini Septemba 19 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kazi ya kuwahudumia watanzania.

Breaking News: Chadema watangaza kuahirisha UKUTA kwa mwezi mmoja
Christian Benteke Afunguka, Asema Klopp Alishindwa Kumuelewa