Serikali kupitia wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi imetoa wito kwa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kutoa elimu kwa wananchi ili wakubali kulipwa fidia na kuliachia ‘shamba la Somji’.

Naibu waziri wa wizara hiyo, Angelina Mabula ameyasema hayo leo bungeni wakati akijibu swali la Mdee aliyetaka kufahamu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika mgogoro huo ili wananchi waendelee na shughuli zao.

Amesema kuwa Mbunge huyo anapaswa kuwaelimisha wananchi hao kukubali kulipwa fidia na kupisha shamba hilo kwani mmiliki halali ni Hussein Somji na Munaver Somji waliopewa hati ya umiliki tangu mwaka 1961 inayodumu kwa miaka 99.

Kwa mujibu wa Mabula, awali shamba hilo lilikuwa na ukubwa wa ekari 366, lakini lilimegwa kwa matumizi mahsusi ya Serikali mwaka 1975 na mwaka 2002.

Alisema kuwa endapo wananchi hao hawatapewa elimu ya kukubali kufanya mazungumzo na Serikali ili wapewe fidia na kukubali kupewa maeneo mengine, Serikali itatekeleza uamuzi wa Mahakama kuwa wananchi hao ni wavamizi hivyo wanapaswa kuondolewa.

Swali la Mdee liliulizwa bungeni kwa niaba yake na mbunge wa Liwale kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Zuberi Kuchauka.

Mdee ambaye aliwasili nchini akitokea Afrika Kusini kwa matibabu, hakuwepo bungeni.

Miili ya Wanajeshi wa Uganda yawasili nchini humo
John Heche kupandishwa kizimbani