Serikali imesema kuwa haitaruhusu vyombo vya nje kuingia nchini kwa ajili ya kuchunguza sakata la kutekwa kwa bilionea Mohammed Dewji kwani ni suala ambalo liko ndani ya uwezo wa vyombo vya ndani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema kuwa Jeshi la Polisi lina wataalam ambao wana uwezo na weledi wa kuweza kushughulikia suala hilo.

“Kuna haja gani ya kuleta vyombo vya nje wakati tuna jeshi bora na lenye uelewa mkubwa licha ya kukabiliwa na changamoto za hapa na pale,” Masauni anakaririwa.

Kauli hiyo ya Masauni imekuja wakati ambapo waziri kivuli wa mambo ya ndani, Godbless Lema akizungumza na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine aliitaka Serikali kuruhusu vyombo vya nje kuchunguza sakata hilo.

Familia ya Mo Dewji ilitangaza zawadi ya Sh1 bilioni kwa mtu atakayetoa taarifa itakayosaidia kupatikana kwa mwanafamilia wao aliyetekwa na watu wasiojulikana Oktoba 11 mwaka huu  jijini Dar es Salaam.

Jeshi la polisi liliwakamata watu 26 kwa ajili ya uchunguzi wa sakata hilo, hadi sasa watu 19 wameachiwa kwa dhamana.

Video: Lema afunguka kuhusu 'Mo Dewji' ataka wachunguzi wa Kimataifa
Amteka mama wa mpenzi wake baada ya mwana kumsaliti