Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeandaa mafunzo maalum kwa walimu 800 kutoka halmashauri 20 nchini ikiwa na lengo la kukuza kiwango cha ufaulu hasa katika somo la Hisabati na Sayansi

Kwa mujibu wa mwezeshaji kutoka chuo kikuu cha Dodoma (UDOM), Dkt. Alfred Hugo amesema mbali na mambo mengine pia mafunzo hayo yanayofanyika Jijini hapa kwa siku 14 yanalenga kuwajengea walimu uwezo wa kutambua zana za kufundishia kulingana na mazingira.

“Mafunzo haya ni kwa walimu wa somo la hisabati kwa shule za msingi na upande wa sekondari tumezingatia yale masomo ya sayansi kwani ipo changamoto kubwa ya ufundishaji kwa walimu kwa kutokua na vifaa vya kufundishia,” Amefafanua Dkt. Hugo.

Amesema wakiwa katika mafunzo hayo pia walimu wanafundishwa jinsi ya kuwa wabunifu kwenye ufundishaji ili kuwafanya wanafunzi kufurahia masomo na kutoona ugumu kujifunza hasa kwenye masomo ya sayansi na hisabati.

Naye mmoja wa walimu walioshiriki mafunzo hayo kutoka Shule ya Msingi Banguma iliyopo Wilayani Chemba Mkoani Dodoma, Nuru Mwendalile ameishukuru Serikali kwa kusema anaamini yatakua msaada kwao pindi watakaporudi katika maeneo yao ya kazi kufundisha.

“Kiukweli tunaishukuru Serikali kwa kutuletea fursa hii maana katika Wilaya yetu kuna changamoto za ufaulu lakini tunaamini baada ya kupata mafunzo haya tutayatumia kuboresha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule zetu,” amebainisha Bi. Mwendalile.

Mafunzo hayo yaliyoanza Desemba 10 yanaratibiwa na wizara kupitia mradi wa uwezeshaji wa elimu (TESP) kwa kushirikiana na ubalozi wa Canada ambapo katika halmashauri 20 zilizoshirikishwa shule za Msingi ni 8 na Sekondari zikiwa 12 na yanatarajia kuhitimishwa rasmi Desemba 23, 2019.

Mabadiliko TEHAMA yahitaji mafunzo ya usalama wa mitandao
Video: Wingu zito kukamatwa Magoti wa LHRC, mamia ya abiria wakwama Ubungo