Serikali nchini Rwanda, imeongeza mishahara ya Walimu wa shule za msingi, ambao sasa watapata nyongeza ya asilimia 88 ya mishahara yao kuanzia mwezi huu wa Agosti 2022, ikiwa ni sehemu ya motisha inayolenga kuboresha maisha yao.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya elimu ya nchi hiyo, iliyotolewa kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter Agosti 1, 2022 imesema chini ya marekebisho hayo mapya, walimu wa shule za upili pia watapata nyongeza ya malipo ya ongezeko la asilimia 40.

Aidha, taarifa hiyo ilibainisha kuwa mishahara halisi ya walio na cheti katika taaluma ya ualimu ambayo kwa sasa inaanzia 50,849 FRW (sawa na Tsh.114,472.22) na itapanda hadi Tsh. 215,221.86.

“Mishahara ya Walimu Wakuu, Manaibu Walimu Wakuu, na wafanyakazi wasaidizi katika shule za Umma na zinazosaidiwa na Serikali, pia imerekebishwa na kuwekewa ongezeko na maamuzi haya yanaanza kutekelezwa kutokana na malipo ya mishahara ya walimu ya Agosti 2022,” imesema taarifa hiyo.

Ingawa Rwanda imeongeza mishahara ya walimu kwa asilimia 10 tangu Machi 2019, gazeti la The New Times la nchi hiyo linaripoti kwamba zaidi ya walimu 1000 huacha taaluma yao kila mwezi ili kutafuta ustawi bora.

Nyongeza hiyo mpya ya mishahara, ni sehemu ya mpango utakaojumuisha motisha ya kuboresha maslahi ya Walimu na kukuza ubora wa elimu katika shule za umma na zinazosaidiwa na Serikali kwa elimu ya jumla na TVET.

Sita wakamatwa ulaghai wa tovuti mapenzi ya jinsia moja
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo August 4, 2022