Serikali imepanga kuajiri walimu 11,000 wa shule za msingi na sekondari katika mwaka wa fedha wa 2017/18.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jafo amesema katika mpango huo, walimu 7, 000 watakuwa wa shule za msingi na 4,000 wa sekondari na kuongeza kuwa hadi kufikia Desemba 31, walimu 2,700 watakuwa wameshaajiriwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma wakati wa kurekodi kipindi cha Tujadiliane kinachoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kurushwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari, Jafo amesema ajira hizo zitapunguza upungufu wa walimu unaotokana na ongezeko la wanafunzi tangu Sera ya Elimu Bure ya Msingi ianze kutekelezwa.

Tangu mwaka jana, Serikali inatekeleza sera hiyo inayoligharimu Taifa zaidi ya Sh20 bilioni kila mwezi, huku idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa katika shule za msingi na wale wanaojiunga na za sekondari ikiongezeka kwa zaidi ya wanafunzi milioni moja.

Hata hivyo, Jafo aligusia miundombinu shuleni na kusema kuwa  Serikali imetenga zaidi ya Sh37 bilioni za ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari za umma 148.

Ameongeza kuwa zaidi ya Sh21 bilioni zimetumika kujenga mabweni 85 katika awamu ya kwanza ya mpango huo, huku awamu ya pili ya kujenga mabweni 65 iliyoanza kutekelezwa Agosti ikitarajiwa kugharimu Sh16 bilioni.

Pia amesema Serikali imetenga zaidi ya Sh246 bilioni kukabiliana na upungufu wa matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa katika shule za umma.

“Theluthi moja ya fedha hizo, sawa na Sh82 bilioni zitatumika kukamilisha miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo inayotekelezwa kwa nguvu za wananchi,” amesema Jafo.

Video: Tamasha la RC Makonda lafanyika jijini Dar

Comments

comments