Serikali imetangaza kuwa wamepata mwendeshaji wa pili wa mradi wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (DART) anayejiita Emirates kutoka Dubai na siku za karibuni wataanza kuingiza mabasi yao yaendayo kasi  baada ya mwendeshaji wa kwanza wa mradi huo, Kampuni ya Uda-Rapid Transit (Uda-RT), kuonekana kusuasua.

Hata hivyo uchache wa mabasi yanayotumika katika mradi huo kwa sasa yameelezwa kutotosheleza, jambo linalosababisha msongamano vituoni na katika mabasi.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege, amesema ili kumaliza kero hizo, tayari kandarasi imeshatangazwa na mwendeshaji mpya ameshapatikana.

“Kandarasi imeshatangazwa na ameshapatikana mmoja anayejiita Emirates kutoka Dubai, nao wataingiza mabasi yao.

“Siwezi kusema ni lini ataanza kuingiza mabasi na kuendesha mradi kwa sababu taratibu za zabuni zipo kwenye ‘ku-award’, ila niwahakikishie tunakwenda vizuri. Kuna mambo machache  ambayo hayajawa ‘confirmed’ (thibitishwa).

“Jambo la msingi ni kuhakikisha tunapata ‘operator’ (mwendeshaji) mzuri ili wananchi wa Dar es Salaam waendelee kufurahia usafiri mzuri,” alisema.

Alisema uendeshaji wa mradi huo kwa sasa ni wa awamu ya kwanza, ambao unafanywa na Kampuni ya Uda-RT inayomilikiwa kwa ubia na Kampuni ya Simon Group na Serikali.

Aliyekuwa Katibu Mwenezi CCM auawa kwa kupigwa risasi
Serikali kumwaga ajira za Walimu shule za msingi