Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imepiga marufuku uchapaji holela wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia kwa wachapaji binafsi na badala yake uchapaji huo utasimamiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) ili kuthibiti ubora.

Majaliwa amesema hayo leo Desemba 2, 2016 wakati akizungumza na walimu wa halmashauri ya Jiji la Arusha na wilaya ya Arusha kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani Arusha ambapo amesema mbali na kudhibiti wa ubora pia uamuzi huo unalenga kuwa na kitabu kimoja kwa kila somo kwa kila mwanzfunzi kwa nchi nzima ili kuweka uwiano mzuri katika ufundishaji na upimaji wa wanafunzi.

Ziara hiyo ya Waziri Mkuu inalenga kukagua utelelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Utendaji wa Serikali, kusikiliza na kujionea kero zinazowakabili wananchi  wa Mkoa huo kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa ili kuweza kuzitafutia suluhisho.

Amesema kipindi cha nyuma vitabu vilikuwa vinachapwa na watu mbalimbali hivyo kusababisha malalamiko makubwa kutokana na vitabu hivyo kuwa na makosa mengi. “Sasa vitabu vikibainika kuwa na makosa tutaibana Taasisi ya Elimu Tanzania,”.

Pia ameeleza kuwa Serkali itahakikisha kila mtoto anakuwa na kitabu chake ili kuwawezesha kusoma vizuri na kuwa na uelewa wa kutosha ikiwa ni pamoja na kuwarahisishia walimu katika ufundishaji.

Aidha, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu madeni ya walimu, ambapo  amewataka Wakurugenzi wa  Halmashauri zote nchini kutenga fedha katika mapato yao kwa ajili ya kulipa madai ya watumishi mbalimbali katika maeneo yao wakiwemo walimu.

 

JPM aridhia ombi la Mkuu wa Magereza, amteua Dk. Malewa kuwa Kaimu Mkuu
Lema agonga mwamba tena