Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeshauri Serikali kuandaa mpango Mkakati wa haraka wa kunusuru Ziwa Manyara ambalo liko hatarini kutoweka kutokana shughuli za kibinadamu.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Murad Sadick ambapo amesema kuwa ni wakati muafaka sasa jambo hilo kupewe kipaumbele ili kunusuru hali ya sasa inayotishia uhai wa ziwa hilo.

Wakiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Manyara, Kamati hiyo imetembelea Ziwa Manyara na kujionea kupungua kwa kina cha maji kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kilimo kisicho endelevu hususani katika vyanzo vya maji kinachopelekea ziwa hilo kujaa tope pamoja na ongezeko la mimea vamizi.

“Sote tumejionea hali halisi, hali ni mbaya, mimi na Kamati yangu tunawajibu wa kuishauri Serikali, hatua za haraka na za maksudi kunusuru hali hii, hata kwa maziwa mengine pia kama Ziwa Jipe na Ziwa Chala. endapo hatua za haraka hazitachukuliwa ndani ya miaka kumi ijayo Ziwa hili litatoweka,”amesema Sadick

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), William Mwakilime amesema kuwa Ofisi yake imechukua hatua za makusudi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa Umma juu ya namna bora ya kuwa na kilimo endelevu kinachozingatia matumizi bora ya ardhi na kujenga mabwawa maalumu kwa ajili ya kuchuja maji.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muugano na Mazingira, January Makamba amesema kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha andiko jumuishi litakalogusa sekta zote kwa kuwa ni suala mtambuka na kuahidi kuwa Serikali inalipa uzito jambo hilo kwa mustakabali wa nchi na ustawi wa wananchi wake.

Hata hivyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira iko katika ziara ya kikazi Mkoani Arusha pia itatembelea miradi ya uchimbaji wa visima Bagamoyo Mkoa wa Pwani, ikiwa ni miongoni mwa miradi inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais chini ya Mkataba wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Mbowe afunguka ya Lowassa kurudi CCM, amtaka aseme ukweli
Magaidi waua watu 49 wakifanya ibada msikitini

Comments

comments