Serikali kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano) imetahadharisha kuwa mito mikuu nchini inaweza kukauka ndani ya miaka 15 ijayo, endapo wananchi wataendelea kuharibu vyanzo vya maji.

Akitoa tamko la Wizara hiyo jana jijini Dar es Salaam, katika kuelekea maadhimisho ya wiki ya Mazingira itakayoanza Juni 1 na kufikia kilele chake Juni 5, mwaka huu yenye kauli mbiu ‘Tuhifadhi Vyanzo vya Maji kwa Uhai wa Taifa letu’, Waziri wa Wizara hiyo, January Makamba aliitaja mito hiyo mikubwa kuwa ni pamoja na Rufiji, Pangani na Ruaha.

“Tukiendelea na mwenendo huu wa uharibifu wa vyanzo vya maji na mito, mito yetu mikuu hapa nchini, kama vile Rufiji, Pangani, Ruaha na mingineyo, ambayo inategemewa sana kwa uhai na ustawi wa Watanzania wengi itakauka ndani ya miaka 15 ijayo,” alisema Makamba.

Alisema kuwa kauli mbiu ya maadhimisho hayo pamoja na shughuli zitakazofanyika zinalenga katika kuihamasisha jamii kutofanya shughuli zenye uharibifu wa vyanzo vya maji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba,akiongea na waandishi wa Habari kuhusu Tamko la Siku ya Mazingira Duniani

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba,akiongea na waandishi wa Habari kuhusu Tamko la Siku ya Mazingira Duniani

Akitoa muelekeo wa jinsi maadhimisho hayo yatakavyofanyika nchini, alisema kuwa hakutakuwa na maadhimisho ya kitaifa na badala yake Wakuu wa Mikoa watafanya maadhimisho hayo kwa ngazi za mikoa kupitia muongozo uliotolewa na wizara hiyo. Alisema muongozo huo umeeleza shughuli zitakazofanyika ambazo zitaleta hamasa kwa jamii katika kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji.

Katika hatua nyingine, Waziri Makamba alieleza kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii imefanya makadirio ya kutumia kiasi cha shilingi bilioni 105.2 kugharamia utekelezaji wa mkakati wa miaka mitano (2016 -2021) wa kupanda na kuhifadhi miti nchini.

“Tumetenga shilingi bilioni 2 kama kianzio kwa ajili ya mkakati huu. Tunategemea kwamba baada ya bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha kukamilika, Mfuko wa Taifa wa Mazingira utatengewa vyanzo vya mapato yanayokadiriwa kufikia shilingi bilioni 100, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kifedha ya kugharamia mpango huu na mipango mingine ya hifadhi ya mazingira,” alisema.

Makamba alisema kuwa lengo la mkakati huo ni kuhakikisha nchi inakuwa ya kijani kwa upandaji miti na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.

Mkakati huo pia utawafikia wananchi katika ngazi ya nchini kwa kushindanishwa shule, kata na wilaya zitakazofanya vizuri katika upandaji miti na zawadi nono itatolewa kwa washindi.

Katika ngazi ya kimataifa kwa mwaka huu maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanafanyika nchini Angola yakiwa na kauli mbiu ya ‘Go Wild For Life’.

Kocha Wa Uturuki Amtuhumu Luis Enrique Na Watu Wake Wa Barca
Borussia Dortmund Wakanusha Kuondoka Kwa Aubameyang