Serikali nchini, imesema inafuatilia kwa karibu magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwemo Surua na Rubella kutokana na ongezeko la watu wenye dalili za homa na vipele vinavyohusishwa na ugonjwa wa surua ambao hadi sasa idadi ya wagonjwa waliothibitika imefikia watano.

Hayo, yamebainishwa hii leo Septemba 15, 2022 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu jijini Dodoma wakati akiongelea kuhusu uwepo wa ongezeko la wagonjwa wa Surua nchini bada ya wahisiwa kuchukuliwa sampuli zilizopelekwa maabara ya taifa ya afya ya jamii kwa ajili ya uchunguzi.

Amesema, majibu ya vipimo kwa kipindi cha Julai hadi Agosti umeonesha maeneo saba yana mlipuko wa ugonjwa wa Surua ambapo wagonjwa 38 walithibitika katika Halmashauri za Handeni (4), Bukoba (3), Mkuranga(4) Kilindi (3) na Manispaa ya Kigamboni (8) na kutoa idadi hiyo ya wagonjwa.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dodoma hii leo Septemba 15, 2022 kuhusu kuibuka Kwa ugonjwa wa Surua.

Nyingine ni Manisapaa ya Ilala Sampuli (4), Manispaa ya Temeke sampuli (12), huku akisema mlipuko wa ugonjwa huo huthibitika pale ambapo sampuli tano za wahisiwa huchukuliwa kutoka katika Wilaya moja ndani ya mwezi mmoja na endapo sampuli tatu au zaidi kati ya tano zilizochukuliwa zimetoa majibu chanya.

Waziri Ummy amesema, kulingana na uchambuzi huo kulionyesha uwepo wa ugonjwa wa Surua usiokidhi katika Halmashauri za Arusha (1), Chalinze (2), Igunga(1), Kahama MC (1), Kalambo(1), Kigoma DC (2), Kwimba DC(1), Masasi TC (1), Mvomero DC (2), Rorya DC(2) na Manispaa ya Ubungo (2).

Amesema, “kati ya wagonjwa 54 waliothibitika kuwa na Surua, wagonjwa 48 walikuwa na umri usiozidi miaka 15 na wagonjwa sita walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 15 na hatua za kuuthibiti ugonjwa huo kuwa ni kuimarisha ufuatiliaji wa wahisiwa na tetesi katika ngazi ya jamii.”

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa akishiriki kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio ya matone kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Aidha, amesema njia nyingine ni kutuma timu kwenda maeneo yaliyo athirika zaidi pamoja na kutoa elimu kwa watoa huduma za afya na jamii kuhusu dalili na jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo, huku akitoa rai kwa jamii kupeleka watoto kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wapatiwe chanjo ya Surua.

Awali, Mkurugenzi wa huduma za Kinga wa Wizara ya afya, Dkt. Beatrice Mutayoba alisema dalili za ugonjwa wa surua ni pamoja na homa ya vipele inayoweza kuambatana na kikohozi, mafua, macho kuwa mekundu na vidonda mdomoni.

Ameongeza kuwa, ugonjwa huo hauna tiba maalum na kwamba usipodhibitiwa mapema huleta madhara kwenye masikio, na wakati mwingine hupelekea homa ya mapafu, upofu wa macho, homa ya uti wa mgongo au kupoteza maisha.

Uhuru vyombo vya Habari: Demokrasia yazidi kudidimia
Rais Zelensky ayaweka maisha yake rehani