Serikali imeyafuta mashamba sita yenye ukubwa wa hekari 12,915.126 ya kampuni ya Mohamed Enterprises yaliyopo korogwe mkoa wa Tanga.

Uamuzi wa kufuta mashamba hayo unafuatia mapendekezo yaliyotolewa na halmashuri ya wilaya ya Korogwe kufutwa mashamba hayo kutokana na kutoendelezwa kwa muda mrefu na baadaye maombi hayo kuwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wizara kwa nia ya kufutwa.

Mashamba yaliyofutwa ni yale yaliopo eneo la Mombo, Mabogo pamoja na Kwalukonge wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Akizungumza mara baada ya kutembelea mashamba hayo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.  Angeline Mabula amesema kuwa mashamba yaliyobatilishwa ni kati ya mashamba 14 yanayomilikiwa na kampuni ya Mohamed Enterprises Mazinde wilayani Korogwe na kubainisha kuwa uamuzi huo unalenga kujenga nidhamu kwa waliopewa rasilimali za serikali kuzingatia masharti ya uwekezaji.

Amesema kuwa mara baada ya halmashauri ya wilaya ya Korogwe kupeleka mapendekezo ya kufutwa mashamba ya Mohamed Enterprises, wizara ya ardhi ilifanya ufuatiliaji juu ya maombi ya halmashauri husika la kutoendelezwa mashamba na baada ya kujiridhisha ikawasilisha maombi hayo kwa rais na kuridhiwa.

Katika uamuzi huo wa Rais kuridhia ubatilishaji mashamba sita kati ya 14 yanayomilikiwa na Mohamed Enterprises unalenga kuhakikisha wote waliopewa maeneo kwa ajili ya uwekezaji wanazingatia masharti na taratibu za uwekezaji.

Hata hivyo, Dkt. Mabula amesema kuwa mashamba ambayo hayajabatilishwa yamewekewa utaratibu kwa nia ya kuyaboresha kwa kuwa baadhi yake yanahitaji maboresho kwa nia ya kufanya vizuri.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Tanga Martin Shigela amewataka wananchi wa Korogwe kutovamia maeneo ya mashamba yaliyobatilishwa hadi hapo Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe itakapopanga matumizi bora ya ardhi katika mashamba hayo.

 

Kim Kardashian athibitisha ujio wa mtoto wa nne
SADC yaikaba koo CENI, yataka kura zirudiwe kuhesabiwa Congo DR