Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imesema haina mpango wa kuwarejesha nchini wanafunzi 420 waliopo mji wa Wuhan nchini China kwa kuwa nchi zilizofanya hivyo zilisababisha kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona katika nchi husika.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jana, inaeleza kuwa haifikirii kuwarejesha wanafunzi hao nchini na imewatoa hofu kuwa inaendelea kufuatilia hali zao kwa karibu.

Imesema hadi sasa hakuna mwanafunzi au Mtanzania yeyote aliyebainika kuambukizwa virusi hivyo na kuwasihi kuendelea kuwa watulivu.

“Wizara inapenda kuuhakikishia uma kwamba Serikali ya Tanzania haina mpango wa kuwaondoa ama kuwasafirisha wanafunzi hao walioko Wuhan kwa kuwa wako katika uangalizi maalum (quarantine) nchini humo,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa wizara hiyo, Emmanuel Buhohela.

Imesema kutokana na kuheshimu masharti na mahitaji ya karantini hiyo yanayozuia mtu yeyote kutoka ama kuingia katika mji huo kwa kusudi la kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo hadi hapo Serikali ya China itakapoondoa karantini hiyo.

 “Serikali pia inakamilisha mpango wa mawasiliano ya moja kwa moja kwa njia za simu (hotline) zitakazotumiwa na wataalamu wa saikolojia (psycho-social support) kwa ajili ya kuwapatia ushauri nasaha wanafunzi na wazazi wakati juhudi za kudhibiti mlipuko huo zikiendelea,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kisiwa chote cha Zanzibar kupuliziwa dawa ya Malaria
Tamko la Waziri Ummy wanafunzi kutibu wagonjwa Mloganzila