Wananchi Mkoani Arusha, wametakiwa kufika Mahakamani ili kutoa ushahidi wa matukio ya ukatili wa kijinsia, yanayotokea katika maeneo yao baada ya kuripotiwa katika vituo vya Polisi.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa ameyasema hayo Machi 25, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Sekei iliiyopo Jijini Arusha, waliojitokeza katika mkutano uliondaliwa na Umoja wa Wanawake wa kata hiyo, kwa ajili ya kupinga vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji na ulawiti.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa.

Amesema, baadhi ya wananchi wamekua na tabia ya kumaliza kimya kimya matukio ya ukatili yaliyotokea katika jamii zao, kwa kupewa hela ama kuahidiwa zawadi ikiwa wataacha kwenda kutoa ushahidi Mahakamani au kuacha kuyaripoti.

Mtahengerwa amebainisha kuwa, Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika katika kupanga njama za kukwamisha kesi za ukatili, katika Jiji la Arusha.

Sehemu ya Wananchi waliojitokexa kuhamasisha mapambano dhidi ya ukatili Mkoani Arusha.

Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Arusha, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Happiness Temu amesema kupitia mkutano huo wananchi wamepata elimu juu ya ukatili, aina za ukatili, madhara ya ukatili na umuhimu wa kuwahi kuripoti matukio ya ukatili.

Amesema, ili kumaliza matukio ya ukatili ni lazima jamii yote kuwa na ushirikiano wa pamoja wa kukemea vitendo hivyo badala ya kuliachia jeshi la Polisi pekee.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Arusha, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Happiness Temu.

Nao baadhi ya wanawake wa Kata hiyo, wamesema wameandaa mkutano huo ili kuhamasisha jamii kuungana na kukemea vitendo vya ukatili ambavyo vimekua vikiongezeka.

Mama Janeth Magufuli atunukiwa Tuzo ya Heshima
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Machi 26, 2023