Serikali imetoa wito kwa Vyama,Vilabu na Mashirikisho ya mpira wa miguu kuzingatia na kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa katiba zao ili kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza katika uendeshaji na uendelezaji wa soka nchini.
Hayo yamesemwa Leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia Wambura  wakati akijibu swali la Mhe. Khatibu Saidi Haji Mbunge wa Konde (CUF) kuhusu makosa yanayofanywa na  klabu za soka nchini kwa kupeleka mambo ya kisoka katika mahakama  ambapo ni kinyume cha sheria za FIFA.
Mhe. Annastazia Wambura amesema ni kweli kuwa Sheria za FIFA zinakataa mambo yanayohusiana na soka kupekekwa mahakamani hivyo hatua hiyo ya Vyama na Klabu kuzingatia Sheria na taratibu inalenga kuwezesha masuala ya soka kuendeshwa kwa  kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa na Mamlaka za Michezo huo kwa ngazi mbalimbali.
Aidha amesema hatua hiyo imewezesha mchezo wa soka kuchezwa na kupata  matokeo kwa wakati na hivyo kuepusha mazuio ya mahakama ambayo yanaweza kusababisha usumbufu usio wa lazima kwa washiriki wengine hata kupelekea kufungiwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF).
Maendeleo ya michezo hapa nchini yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo ya mwaka 1967, kama ilivyorekebishwa kwa mujibu wa Sheria Na 6 ya mwaka 1971 lakini bado  Sheria hii inakinzana na Sheria za FIFA ila serikali inafanya mapitio ya Sheria hiyo ili iendane na wakati kwa lengo la kuboresha na kuendeleza michezo nchini.

Luis Suarez Bado Ana Ndoto Za Kurejea Anfield
Breaking News: Vurugu zaibuka bungeni jioni hii