Serikali, imesema sababu za wananchi kujichukulia sheria mikononi na kupelekea kuongeza kwa wimbi la mauaji nchini zinatokana na wivu wa mapenzi, migogoro ya ardhi, ulevi na imani za kishirikina.

Akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani hii leo Septemba 14, 2022 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Hassan Chande, amesema katika kudhibiti hali hiyo waliunda timu maalumu ya kuchunguza na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua.

Amesema, pamoja na kuchukua hatua za kisheria kama zilivyopendekezwa na timu waliyoiunda, Serikali kupitia Jeshi la Polisi pia imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo uzingatiaji wa sheria.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tulia Akson.

Chande ameongeza kuwa, elimu hiyo imekuwa ikitolewa  kwa kuwashirikisha viongozi wa siasa, dini, wazee wa mila na watu wanaoheshimika kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi, katika kutatua migogoro na migongano katika jamii.

Kufuatia majibu hayo, Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson amesema licha ya Serikali kuchukua hatua bado tatizo hilo linaendelea kukua, hivyo akaitaka Serikali kuangalia hatua za ziada.

Amesema, “Na mtuulize sisi watu wa kawaida kabisa tunafikiri hilo jambo linaweza kumalizwa kwa namna gani kwasababu kadri linavyozungumzwa utasikia leo huku, kesho huku, sasa huenda linatembea kwasababu linazungumzwa na watu wazito.”

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Hassan Chande.

Naye, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, George Simbachawene amesema iko haja ya kushirikiana na wadau,katika kukabiliana na changamoto hiyo.

Amesema, “Law enforcers (wasimamizi wa sheria), tujiulize tunatimiza wajibu wetu sawa sawa, kama kunatokea hasira ya wananchi kuchukua hatua mkononi kwanini wanachukua hatua mkononi? Ni wapi hapako sawa.”

Awali, Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso alitaka kufahamu nini kauli ya Serikali katika kutatua changamoto ya wimbi kubwa la mauaji, nchini Tanzania.

Waombolezaji waonywa ufikiaji mwili wa Malkia
Idadi wanaoishi kwenye ndoa na kazi za kulazimishwa yatisha