Serikali imetoa notisi ya siku 24 kwa wamiliki wa machapisho (magazeti na majarida) ambayo bado hayajahuisha leseni zao kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kuhakikisha wanahuisha leseni hizo hadi ifikapo Machi 21, 2019 vinginevyo hayataruhusiwa kuchapishwa.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa masuala mbalimbali ya Serikali ikiwemo utekelezaji wa Sheria ya Huduma ya Habari.

Amesema kuwa, utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari unaendelea hivyo wakati wowote kuanzia sasa chombo cha kwanza cha kusimamia wanahabari yaani BODI YA ITHIBATI itaundwa ambapo kazi yake kubwa ni kusajili wanahabari, kuwapa vitambulisho vya kitaaluma na kusimamia maadili yao.

“Kwa mujibu wa Sheria mpya ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016, wamiliki wote wa magazeti na majarida wanapaswa kuhuisha leseni zao kila mwaka na tulitoa notisi kwa ambao hawajahusiha, wapo walioitikia wito na wapo waliokaidi, orodha kamili imewekwa katika www.maelezo.go.tz” amesema Dkt. Abbasi.

Aidha, amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa Waandishi wa Habari wanatekeleza majukumu yao bila vikwazo na pia wananchi wanapata taarifa mbalimbali, Dkt. Abbasi ametoa wito kwa Watendaji mbalimbali wa Serikali katika ngazi zote kutoa habari na kueleza utekelezaji wa ahadi mbalimbali za Serikali kwani ni takwa la Katiba na Sheria.

Hata hivyo, Dkt. Abbasi ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza kwa kasi wajibu wake kwa umma ikiwemo kuhakikisha hali ya amani, utulivu, kusimamia utawala bora na utawala wa sheria.

JPM azidi kung'ara Kiuchumi na Utawala bora barani Afrika
Nicki Minaj, Cardi B waungana kumtetea rapa wanayempenda