Serikali imeunda timu ya wataalamu inayoendelea na kazi ya kutatua na kupatia suluhisho la migogoro mbalimbli ya ardhi nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Kamani alipokuwa akijibu swali la Mhe. Dkt Shukuru Kawambwa lililohusu mpango wa Serikali katika kumaliza mgogoro kati ya TANAPA na vitongoji vya Kitame, RAZABA Gama-Makani katika kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo.

Mhandisi Kamani amesema kuwa mgogoro baina ya kijiji cha Makarunge na hifadhi, unaonesha wananchi hawakushirikishwa katika zoezi la uwekaji mipaka ambapo zoezi hilo liliwashirikisha kikamilifu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa mkutano na wanakijiji hao.

Aidha, Mhandisi Kamani amesema kuwa mgogoro wa baina ya shamba la RAZABA na hifadhi umetokana na utata wa eneo la takribani hekta 3,441, ambapo juhudi za kutatua mgogoro huo zinaendelea kufanyika kwa kushirikisha ngazi za vijiji, wilaya, mkoa na wizara husika na kutolewa maelekezo ikizingatia athari za mazingira.

Kwa upande wa mgogoro baina ya Gama-makani na hifadhi, Mhandisi Kamani amesema kuwa mgogoro huo unatokana na malalamiko ya wananchi kuwa baadhi yao walifidiwa wakati wa uanzishwaji wa hifadhi ambapo hawakuwa wamiliki wazawa wa maeneo hayo.

“Mgogoro huu unatokana na malalamiko ya wananchi kuwa baadhi ya wananchi ambao walifidiwa wakati wa uanzishwaji wa hifadhi katika eneo hilo, hawakuwa wamiliki wazawa wa maeneo hayo, ingawa taarifa zinaonesha kuwa mchakato wa malipo ya fidia ulifuata taratibu muhimu ikiwemo ushirikishwaji wa karibu wa uongozi wa wilaya ya Bagamoyo, Serikali za kata na Serikali za vijiji husika,” amefafanua Naibu Waziri huyo.

Migogoro yote iliyoainishwa inahusiana na hifadhi ya taifa Saadani iliyoanzishwa kisheria kwa tangazo la serikali (GN) Na. 281 la mwaka 2005

Wilaya ya Mbozi Kuendelea Kunufaika na Kivutio cha Kimondo
Mh. Makamba Awataka Wanasiasa Kutoingiza Masuala ya Muungano Kwenye Siasa