Wafanyabiashara wa mkaa nchini, wametakiwa kufuata Sheria za nchi hasa eneo la uhifadhi wa mazingira, kutokana na uwepo wa wimbi la uvunaji wa mazao ya misitu, ukataji na uchomaji wa mkaa usiozingatia sheria, kanuni na taratibu za Serikali.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana, Bungeni jijini Dodoma hii leo Septemba 22, 2022 wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Mbogwe – Geita, Nicodemus Maganga, wa CCM.

Amesema, “Inapotokea mwananchi anasafirisha mazao ya misitu (mkaa), bila kufuata utaratibu, mazao hayo hutaifishwa na Serikali, uvunaji holela wa mkaa umesababisha kutoweka kwa kasi maeneo ya misitu hali inayosababisha athari za mabadiliko ya tabia nchi.”

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja.

Akizungumzia juu ya askari wa Misitu, wanaodaiwa kuwapiga na kuwanyang’anya mkaa wananchi wa Mbogwe, Masanja amesema Wizara haitosita kuwachukulia hatua watumishi wake wanaohusika na uvunjaji huo wa sheria, kanuni na taratibu na kuwataka Wananchi kutoa taarifa pale wanapofanyiwa vitendo hivyo ili hatua zichukuiliwe.

Awali akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka kuhusu ni lini Serikali itatoa vibali vya Uwindaji, Waziri Masanja amesema vibali vya uwindaji wa kitalii vinaendelea kutolewa kwa mujibu wa kanuni ambapo hadi sasa jumla ya minada saba imefanyika na vibali kutolewa.

Mabalozi wateule, waaswa kuitumia Diplomasia
Makamu wa Rais 'ateta' na Katibu Mkuu wa UN