Serikali imewataka wananchi hususani wakulima wa korosho nchini kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa wa korosho kutoka maeneo mbalimbali duniani ili kupata masoko ya uhakika ya zao hilo.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu bei ya korosho ambayo imeshuka katika msimu wa mwaka huu hadi kusababisha wakulima kugomea baadhi ya minada, ambapo Waziri Mkuu amesema kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na Serikali.

“Tunaendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa ili tujue ni nani atanunua korosho na kwa kiasi gani, hivyo tunawaomba wakulima waendelee kuwa watulivu, Serikali inajitahidi kuhakikisha zao hilo linatafutiwa masoko. Korosho zitanunuliwa tu.”amesema Majaliwa

Aidha, amesema kuwa Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya ujenzi wa viwanda vya mbolea, ambapo inatoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika viwanda vikiwemo vya pembejeo.

Hata hivyo, ameongeza kuwa viwanda vya mbolea vilivyopo nchini ni vichache na havitoshelezi mahitaji, hivyo kwa sasa kuna utaratibu wa kujenga viwanda vingine viwili kimoja kitajengwa Kilwa mkoani Lindi na kingine kitajengwa Mtwara. Kukamilika kwa viwanda hivyo kutaongeza uzalishaji wa mbolea na kupunguza uagizaji kutoka nje ya nchi.

 

 

Humoud arudisha mashambulizi KMC
Ikulu ya Marekani yafuta kibali cha mwandishi aliyejibizana na Trump