Serikali imezindua kituo cha huduma kwa wakulima, ambapo wadau wa kilimo na Wakulima watapata huduma mbalimbali kwa kupiga simu ya bure na kupatiwa taarifa za mambo yanayohusu kilimo.

Kituo hicho cha Huduma (Call Centre), kimezinduliwa jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwa lengo la kuwapatia wakulima taarifa mbalimbali za kilimo, kusikiliza na kutatua kwa haraka changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima kwa kupiga namba ya 0733 800 200 bila gharama.

“Haya ni maelekezo ya Rais, Samia Suluhu Hassan kwamba ni lazima Wizara iwafikie na kuwahudumia wakulima kwa ukaribu mkubwa ili kufikia malengo tuliyojiwekea katika kuikuza sekta hii muhimu ya kilimo,” amesema Bashe.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akiwa katika mitambo ya kituo cha huduma kwa wakulima

Waziri Bashe ameongeza kuwa, hakutakuwa na gharama yoyote kwa mkulima kupiga simu kwa ajili ya kupata taarifa sahihi, na hivyo kuto kwa wakulima kuitumia fursa hiyo.

Aidha, ameongeza kuwa kituo hicho kitarahisisha upatikanaji wa taarifa za kilimo kwa wakati na kutoa taarifa sahihi za kilimo, ili wakulima na wadau wa Kilimo nchini waweze kupiga hatua na kufikia malengo.

Awali, Katibu Mkuu wa Kilimo Andrew Massawe amesema kituo hicho kitaboreshwa kwa miundombinu ya kisasa, ili kiongeze ufanisi katika kuwahudumia wakulima wa Tanzania na kuongeza kuwa Wizara imejipanga kutumia mfumo wa Kilimo Mtandao ili kutoa huduma stahiki.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akielekeza jambo wakati wa uzinduzi wa kituo cha huduma kwa wakulima, aliyevaa kofia ni Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amebainisha mkakati unaotarajiwa kutekelezwa na Wizara hiyo wa uanzishwaji wa Chaneli maalum ya KILIMO kwenye Vituo vya luninga ili kufikisha ujumbe kwa habari za kilimo kwa umma na kwa uharaka.

Collins Opare atimkia Dodoma Jiji FC
Waziri Mkuu 'akalia kuti kavu' mawaziri wake wajiuzulu